![]()
Huduma za kilimo na ufugaji kwenye Kaunti ya Taita Taveta zinatarajia kupigwa jeki. Hii ni baada ya Gavana wa Kaunti hiyo Andrew Mwadime kukabidhi wahudumu wa nyanjani pikipiki spesheli watakazo kuwa wanazitumia kama njia ya usafiri wao.
Pikipiki hizo zimefadhiliwa na shirika la NAVCDP (National Agricultural Value Chain Development Project) kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Taita Taveta.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Gavana Mwadime amesema pikipiki hizo zitaboresha utoaji wa huduma nyanjani.
“Hizi pikipiki zinaenda kusaidia afisaa wetu kuweza kufikia wakulima kwa haraka sababu kumekua na kilio kwamba afisaa wangu hawaonekani mara kwa mara huko nyanjani, sasa nafikiri hicho kilio kinakwenda kuisha,” Mwadime amesema.
Mwadime aidha amechukua fursa hiyo kuwa onya maafisaa hao dhidi ya matumizi mabaya ya pikipiki hizo.
“Nawaombeni tuwe wazalendo wa kaunti hii, tumieni hizi pikipiki kwa malengo yaliyokusudiwa na sio eti kuenda kufanya shughuli zenu tofauti na ile ya kuwahudumia wakulima na wananchi wa kaunti yetu. Msiwe kama wale wanatafuta kazi kwa bidii na wakipata wana anza tena kuinyonya zaidi, hiyo tabia ya kunyonya watu wa achane nayo. Msianze kufikiria vile mko na hiyo pikipiki mtaenda kuiba mafuta ama kuitumia kama bodaboda kufanya shughuli zenu, tusifanye hivyo na tuzingatie kazi tuboreshe hili jimbo.” Gavawa awarai maafisa hao.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo na Ufugaji Erick Kyongo ametoa wito kwa maafisaa hao kuwa makini kazini na kuhakikisha mkulima anapata huduma kwa wakati unaofaa ili kuboresha uzalishaji.
“Tulikuja gundua changamoto kubwa ya wakulima wetu kupata huduma mashinani ni wahudumu wa nyanjani. Walikuwa hawawezi kuwafikia na tukaona kama idara hili ni tatizo ambalo tunapaswa kulipatia kipaombele na kuitatua ili wakulima wapate muduma kama stahiki gavana Mwadime alivyo ahidi” Waziri alieleza.
Ameongeza kuwa pikipiki hizo zimegharimu milioni tisa na zina kwezo wa kutembea pahali popote licha ya njia na barabara za kaunti hii kuwa na milima na mabonde.
“Pikipiki hizi zina uwezo wa kuishi miaka mingi na zinaweza kupanda barabara zetu zote licha ya kuwa na milima na mabonde na wahudumu wetu wametuhakikishia kazi na huduma inaenda kuboreka. Tunachukua fursa hii kama idara kumpongeza Gavana kwa kutupatia ridhaa hiyo ya kuhakikisha kuenda mbele na kutatua tatizo ambalo lilikua ni sugu katika kaunti yetu ya Taita Taveta.” Waziri aliongeza.
Irene Chenga, afisaa wa kilimo katika wadi ya Mboghoni, kaunti ndogo ya Taveta, amepongeza hatua ya serikali kuwawezesha na kurahisisha usafiri wanapohitajika na mkulima shambani. Kauli yake imeungwa mkono na Francis Mzame, afisaa wa mifugo kwenye wadi ya Kaloleni na Sagala, Kaunti ndogo ya Voi.
“Tukipigiwa simu na mwananchi ama kulima inachukua muda kumfikia sababu ya changamoto za usafiri na umbali ambapo yupo. Lakini baada ya kupewa hizi pikipiki sasa ni rahisi kwetu kuwafikia mahali popote walipo kwa haraka na kwa wakati ufaao.” Mzame alisema.
Kilichosalia sasa nikuona maneno yao yakitiwa vitendo kwa manufaa ya mkulima na kuboresha uzalishaji wa chakula.