Loading

Viongozi wa kaunti ya Taita Taveta, wakiandamana na wanaBodaboda na wananchi, walifika katika kituo cha polisi cha Voi wakitaka majibu kuhusu ongezeko la utovu wa usalama unaowalenga wanabodaboda.

Tatizo la uhalifu limewafanya wengi kupoteza pikipiki zao, huku wengine wakijeruhiwa na wengine kuuawa.

Wakiongozwa na mwakilishi wa kike wa kaunti hiyo, Bi. Lydia Haika, Mbunge wa Voi, Hamisi Chômé, Mbunge wa Mwatate, Peter Shake, pamoja na wawakilishi wa wadi mbalimbali, viongozi hao walielekeza lawama kwa idara ya usalama ya Taita Taveta kwa kushindwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya wahalifu wanaowalenga wanabodaboda.

“Tunaona kwamba hatupati haki. Mpaka sasa watu sita wameuawa, lakini hakuna hata mmoja aliyekamatwa. Hili ni jambo lisilokubalika,” alisema Bi. Haika kwa hasira.

Mwakilishi wa Wadi ya Mbololo, Lawrence Mzugha, aliongeza kuwa ukosefu wa ushirikiano kati ya wanabodaboda haupaswi kuwa sababu ya kushindwa kwa polisi kutatua tatizo la usalama.

Alisema, “Hali imekuwa ya kukatisha tamaa na inahitaji hatua za dharura. Hatuwezi kukubali vijana wetu waendelee kupoteza maisha.”

Wanabodaboda waliopo Voi na maeneo ya karibu walionyesha masikitiko yao juu ya uhusiano duni kati yao na maafisa wa polisi wa ngazi za chini, wakisema kuwa hali hiyo inazuia juhudi za kunasa wahalifu.

“Hatuwezi kumfikia kila afisa wa polisi wa chini, lakini tumekuja hapa tukiamini kwamba viongozi wetu watasikilizwa. Tumeumia sana, tumepoteza vijana na pikipiki zetu,” alisema Ilton Mwarimbo, mmoja wa wanabodaboda mjini Voi.

Hata hivyo, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Voi, Ibrahim Dafala, alikanusha madai ya uzembe na badala yake akaelezea umuhimu wa ushirikiano kati ya polisi na jamii. Alihimiza wanabodaboda kushirikiana kwa kutoa taarifa muhimu zitakazosaidia kurejesha usalama.

“Hakuna taarifa yoyote ambayo imetufikia na tukashindwa kuifanyia kazi. Bila ushirikiano, hatuwezi kujua kinachoendelea. Namba yangu ya simu iko wazi muda wote, mtoe taarifa za maana,” alisema Dafala.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

WhatsApp