![]()
Zaidi ya miaka miwili imepita tangu kutokea kwa ajali mbaya eneo la Taru katika barabara kuu ya Nairobi-Mombasa, lakini bado mayatima kumi kutoka kijiji cha Mgeno, eneo bunge la Mwatate, kaunti ya Taita Taveta, wanakabiliwa na changamoto za kugharamia elimu yao licha ya ahadi za viongozi kusaidia masomo yao zilizotolewa wakati wa mazishi ya wazazi wao mwaka 2022.
Hata hivyo, wanafunzi hawa wamepata afueni baada ya Mwakilishi Wadi ya Mwatate, Joseph Mwalegha maarufu kama Ankoo, kwa kushirikiana na Wakfu wa Joseph Kennedy (JKF), kutembelea kijiji cha Mgeno na kutoa msaada wa zaidi ya shilingi laki moja (100,000) kwa ajili ya karo za wanafunzi hao wa sekondari katika kaunti hiyo.
“Nimeweza kutoa msaada kupitia Joseph Kennedy Foundation kwa watoto hawa ambao walipoteza wazazi wao kwenye ajali, kutimiza ahadi niliyoweka. Natoa cheki za shilingi elfu mia moja na nne ili kuwaunga mkono. Nikiwa niliwachwa yatima nikiwa mdogo, ninaelewa changamoto zao, na ninawaombea wawe na bidii shuleni ili wawe na maisha bora mbeleni,” alisema Ankoo.

Wanafunzi hao, wakiwemo Catherine Shali kutoka Shule ya Wasichana ya Edoro na Dorah Momanyi wa kidato cha nne Mwatate, walionyesha shukrani kwa msaada huo ambao utaweza kupunguza mzigo wa karo na mahitaji mengine ya shule. Waliongeza kuwa hali zao za kifedha ni changamoto kubwa kwa masomo yao, huku wengine wakikosa karo na kulazimika kukaa nyumbani.
Emma Mwongeli, mmoja wa walezi, alieleza ugumu wa kuwatunza wanafunzi hao, akisema kuwa wanahitaji pia msaada wa mavazi na makazi. “Tunamshukuru sana Ankoo kwa msaada wake na tunatarajia wengine wajitokeze kusaidia,” alisema Mwongeli.
Pia, Mchungaji Amon Mdawida wa kanisa la Faith Family, Mgeno, alisisitiza umuhimu wa watu binafsi na mashirika kujitokeza kusaidia mayatima hawa ili kuhakikisha wanapata elimu bora.
Aidha, viongozi wa kaunti waliotoa ahadi za kusaidia wanafunzi hawa wametakiwa kutimiza ahadi zao kwani ‘Ahadi ni Deni.’