![]()
Sherehe za Kitamaduni za Jamii za Taita, Pare na Taveta zinazoishi eneo bunge la Taveta, kaunti ya Taita Taveta, zimezinduliwa rasmi chini ya mwavuli wa DAPATA.
Huu ni ushirika unaozileta pamoja jamii hizi tatu katika kile wamedai kuwa ni hatua ya kuleta utangamano na ushirikiano kupitia kufufua na kutambua utamaduni wao.
Tarehe 10/10/2024, kamati ya DAPATA ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mike Banton na msimamizi wake, aliyekuwa Gavana wa kwanza wa kaunti hii, John Mruttu, iliwezesha uzinduzi wa ushirika huo.
Mamia ya wakazi wa Taveta walihudhuria katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Taita Taveta, eneo la Taveta. Tukio hili pia liliwahusisha viongozi wa serikali kama Katibu Mkuu katika Wizara ya Leba, Shadrack Mwadime, aliyefuatana na viongozi wakuu wa kaunti, wakiwemo Gavana Andrew Mwadime, Seneta Johnes Mwaruma, Mwakilishi wa Kike Lydia Haika, wabunge John Bwire (Taveta), Peter Shake (Mwatate), na Danson Mwashako (Wundanyi).

Wajumbe kadhaa wa Bunge la Kaunti ya Taita Taveta wakiongozwa na Crispus Tondoo walihudhuria, pamoja na viongozi wa zamani kama Thomas Mwadeghu, Johnes Mlolwa, na Mashengu wa Mwachofi. Wazee wa Njavungo wakiongozwa na Ronald Mwasi pia walihudhuria.
Sherehe hizo zilishuhudia uzinduzi wa zoezi la kupanda miti katika Hifadhi ya Watoto Mayatima ya Naima mjini Taveta, ambapo zaidi ya miti 200 ilipandwa.
Hamasa iliendelea kutolewa kuhusu kuendeleza juhudi za upanzi wa miti mara kwa mara ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.
“Napenda kutoa shukrani zangu kwenu nyote kwa kuchagua kuja kupanda miti hapa kwetu. Hatulichukulii tukio hili kwa mzaha bali kwa heshima kuu mliotufanyia, hasa kwa Katibu Shadrack Mwadime, Gavana wetu na Wabunge wetu. Asanteni sana, nasi tutazitunza miti hii ili si kama kumbukumbu tu bali pia kwa kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya baadaye,” alisema Bi Naima, mkurugenzi wa hifadhi hiyo.
Katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Taita Taveta, Tawi la Taveta, sherehe zilianza kwa maonyesho ya vyakula na dawa za kienyeji kutoka kwa jamii hizo, pamoja na densi za kitamaduni, mashairi, na nyimbo mbalimbali kwa lugha za Kitaita, Kipare, na Kitaveta.
Miongoni mwa wasanii waliotumbuiza walikuwa ni Killian Ngure wa wimbo Aba Kwadima na Lalaseri Letashu wa wimbo Haika Papa.
Msimamizi wa DAPATA, John Mruttu, alieleza umuhimu wa utangamano na umoja wa jamii hizo kama mwamko mpya katika kuenzi tamaduni zao.
“Wapendwa, nawashukuru kwa umoja wenu na kufanikisha sherehe hii. Na kama sote tumeona kwamba hili jambo ni jema, tunataka liendelee ili watoto wetu na wajukuu wetu nao wajue mila na desturi zetu. Umoja na kujitolea mliyoonyesha leo yasirudi nyuma,” alisema Mruttu.

Mwenyekiti wa DAPATA, Mike Banton, alihimiza kukumbatia tamaduni na desturi za jamii kama inavyokubalika kikatiba na kusisitiza kuwa siyo ukabila.
Mwakilishi wa wadi, Crispus Tondoo, alitilia mkazo utangamano wa jamii na kudumisha mila zao bila kubaguliwa, akidai kuwa Biblia inawatambua watu kwa kabila. Pia alitoa onyo kwamba DAPATA haitakubali matambiko ya kijadi kufanyika ndani ya Taveta.
“DAPATA hii si kinyume na maandiko matakatifu, kwani hata Biblia inasema kulikuwa na makabila kumi na mawili na Mwenyezi Mungu aliwatambua watu kwa makabila, lakini si kwa ukabila. Tunawaomba ndugu zetu, mambo na matambiko ndani ya Taveta hatutakubali, ila tunataka heshima kidogo tu,” alisisitiza Tondoo.
Kauli za viongozi hao wa DAPATA ziliungwa mkono na wote kwenye hafla hiyo, wakihimiza ushirikiano na utangamano.
Gavana Mwadime aliwarai wawakilishi wa wadi kukubaliana na pendekezo la Wizara ya Masuala ya Utamaduni kutenga bajeti ya shughuli za utamaduni na kuipitisha katika bunge.

Katibu wa Leba Shadrack Mwadime naye alijiunga na viongozi wote na kupongeza mwamko huo mpya, akisisitiza kutumia utamaduni kuboresha uchumi wa kaunti.
“Mambo haya yote ni akili, mipango, na umoja. Hii DAPATA ikitumika vizuri, uchumi wa Taita Taveta utaweza kupanuka, na mtaona utajiri usio na kifani,” alisema Mwadime.
Kwa pamoja, jamii za Dawida, Pare, na Taveta zimeombwa kukumbatia mila na desturi zao na kuahidi kuwa sherehe hizi zitaendelezwa kila mwaka katika maeneo tofauti tofauti.