![]()
Timu ya kandanda ya Mwatate United kutoka Mwatate, Kaunti ya Taita Taveta, imerejea katika ligi ya daraja la pili nchini, NSL. Hatua hii inafuatia ushindi wa kesi mahakamani dhidi ya timu ya Dimba Patriots, ambao walikuwa wameuziwa nafasi ya Mwatate United kwa njia isiyo halali.
Akizungumza na wanahabari, Naibu Katibu wa Mwatate United, Semion Mkala, maarufu kama Sizzo, aliipongeza mahakama kwa kutoa uamuzi wa haki.
Alieleza kuwa timu hiyo iligundua nafasi yao ilikuwa imeuzwa kwa njia ya ulaghai na, licha ya kuwasilisha malalamiko kwa shirikisho, hawakuridhishwa na matokeo. Hivyo, walikata rufaa hadi kwa jopo la kusuluhisha masuala ya michezo, ambalo mwishowe lilitoa uamuzi wa kuwarejesha kwenye ligi.
“Katika msimu wa kifedha wa 2023-2024, tuligundua aliyekuwa mwenyekiti aliuza nafasi yetu kwa njia ya ulaghai kwa Dimba Patriots. Tulifuatilia haki hadi kwa Jopo la kusuluhisha masuala ya michezo, ambalo liliamua nafasi irudishwe kwetu,” alieleza Sizzo.
Shirikisho la soka nchini (FKF) limewafahamisha rasmi Mwatate United kwamba sasa wanaruhusiwa kushiriki ligi hiyo, na hivyo wanatakiwa kuwasilisha stakabadhi rasmi, ikiwemo orodha ya wachezaji, wakufunzi, na uwanja wa nyumbani.
Kutokana na uamuzi huo, Mkala ametoa wito kwa wachezaji kutoka kaunti ya Taita Taveta kujiunga na timu hiyo na kufichua kuwa wanatafuta mkufunzi atakayeongoza timu hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mwatate United, Gamaliel Mwarabu, aliwashukuru wadau wote waliosimama na timu hiyo na kutoa wito kwa wahisani zaidi kujitokeza kusaidia timu katika kukuza vipaji na kuinua uchumi wa jamii.
Michael Kombe, mmoja wa wachezaji walioathiriwa na tukio hilo, alielezea furaha yake kwa kurejea kwa timu hiyo, akisema hali ilikuwa ngumu wakati walipokosa nafasi kwenye ligi. “Ni wakati tena wa kuonyesha kipaji. Tulitegemea hii timu kama ajira, na maisha yalikuwa magumu sana wakati mfereji huo ulikatwa,” alisema Kombe.
Aidha, mashabiki wa Mwatate United, wakiongozwa na Rafael Kimbio, walielezea furaha yao kwa kurejea kwa timu hiyo na kutoa wito kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi kushabikia timu hiyo, wakitaja kuwa mechi hizo huinua uchumi wa Mwatate na Wundanyi.