Loading

Viongozi kutoka Eneo Bunge la Taveta wameitaka serikali ya Kaunti ya Taita Taveta, inayoongozwa na Gavana Andrew Mwadime, kumteua waziri mpya wa Kilimo na Ufugaji kutoka Eneo hilo.

Hii ni kufuatia hatua ya aliyekuwa waziri wa idara hiyo, Eric Kyongo, kujiuzulu wadhifa wake.

Wakiongozwa na Mwakilishi wa Wadi ya Bomeni, Crispus Tondoo, viongozi hao wamesema kuwa Kyongo alikuwa mzaliwa wa Taveta, na hivyo wanahisi ni haki kwa Gavana Mwadime kuteua mrithi wake kutoka eneo hilo.

“Tunasema ya Kaisari mpe Kaisari na ya Mungu mpe Mungu. Bw. Gavana, kama Eric alijiuzulu, si nafasi hiyo irudi Taveta, Mustahiki? Ninajua kuna changamoto nyingi na watu wengi wanaongea na kukusumbua kuhusu nafasi hiyo, lakini kumbuka Eric alitoka Taveta,” alisema Tondoo.

Wakizungumza katika hafla ya kitamaduni mjini Taveta, viongozi hao walimpongeza Kyongo kwa kuwa mchapakazi hodari na mtu aliyeonyesha upendo kwa kaunti hiyo.

“Mustahiki Gavana, kama kuna waziri aliyekuwa mchapakazi na mwenye upendo wa dhati kwako, basi ni Eric Kyongo. Kwa heshima tu! Tunakuomba utimize ahadi yako kwa kutupatia waziri kutoka Taveta,” aliongeza Tondoo.

Aliyekuwa waziri wa kilimo katika Jimbo la Taita Taveta, Erick Kyongo (Kushoto) na Gavana wa Kaunti hiyo, Andrew Mwadime (Kulia).

Kauli hiyo iliungwa mkono na viongozi wengine wa eneo hilo, huku wakisema wanatarajia Gavana ataridhia wito huo.

“Mustahiki Gavana, serikali yako uliitengeneza vizuri kwa kuzingatia uwiano wa mawaziri. Hata hivyo, kwa kuwa kijana wetu Eric alijiuzulu, tunaomba kwa heshima nafasi hiyo irudi Taveta kwa kuwa ni haki yetu kama wakazi wa hapa,” alichangia Halifa Taraya, Mwakilishi wa Wadi ya Mboghoni.

Kwa upande wake, Gavana Mwadime aliepuka kujibu moja kwa moja suala hilo, badala yake akiwataka viongozi kushirikiana kwa karibu katika kuwatumikia wananchi wa kaunti hiyo.

“Uongozi ni ushirikiano. Mnakumbuka maana ya Wakujaa, kuwa ni mtu mwenye amani, upendo na umoja. Tuungane tuwe kitu kimoja na tuachane na fitina. Tuelimishe na kuboresha jimbo letu,” alisema Gavana Mwadime.

Kwa sasa, kutokana na kujiuzulu kwa Eric Kyongo, waziri wa Maji na Mazingira Granton Mwandawiro amekuwa akisimamia wizara ya Kilimo na Ufugaji kwa muda hadi waziri mpya ateuliwe na kuapishwa rasmi.

Aidha, Waziri wa Barabara na Miundomsingi, Martin Tairo, anashikilia majukumu ya wizara yake na yale ya Fedha kwa muda, wakati waziri wa Fedha Danson Katuu akiwa likizoni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

WhatsApp