![]()
Wakazi wa Kijiji cha Bondeni, eneo la Kajire kaunti ya Taita Taveta, wamejitokeza kudai haki baada ya kipande cha ardhi wanachodai kuwa ni chao kuporwa na viongozi wanaosema kuwa eneo hilo ni sehemu ya shule ya msingi ya Kajire.
Wakazi hao wanadai kuwa ardhi hiyo ilikuwa imetengwa kwa maendeleo ya kijamii na wana wasiwasi kuwa watasalia nyuma endapo juhudi zao za kutafuta haki zitaendelea kugonga mwamba.
Katika mkutano uliohudhuriwa na viongozi wa kijiji, wakazi hao wamesisitiza kuwa ardhi hiyo ni mali yao kihistoria na kwamba juhudi zozote za kuwapokonya ni kinyume cha haki.
Wakazi hao pia wamekashifu hatua za maafisa wa polisi kuwakamata vijana wa kijiji hicho wanapofanya maandamano ya amani kutetea ardhi hiyo.
Bwana Wilson Mwaughanga, mmoja wa wazee wa kijiji hicho, alielezea hofu yake kuwa iwapo ardhi hiyo itanyakuliwa, vijana na wakazi kwa ujumla watakosa eneo la kufanyia biashara.

“Sehemu hii ikichukuliwa, basi vijana wetu watakosa eneo la kufanyia biashara zao, hali ambayo itawalazimu kuhama kwenda maeneo mengine,” alisema Bwana Mwaughanga.
Juliana Gombe, mkazi wa eneo hilo kwa takriban miaka arubaini, anadai kuwa serikali ya kaunti imewasahau katika masuala ya maendeleo.
“Wakati vijiji vingine vinapata maendeleo ya kaunti, sisi watu wa Bondeni tunasahaulika; tumechoka kuonekana kama hatufai,” alisema Juliana.
Wakazi wa kijiji cha Bondeni wanaendelea na juhudi zao kutafuta haki katika suala hili huku wakiomba serikali na mashirika ya kutetea haki za binadamu kuingilia kati. Wanasema hawapingi maendeleo ya elimu lakini wanataka uhakikisho kuwa maslahi yao yatatimizwa na hawatadhulumiwa kwa namna yoyote.