![]()
Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa, Kipchumba Murkomen, ametaja migogoro ya ardhi kuwa chanzo kikuu cha ukosefu wa usalama katika Kaunti ya Taita Taveta.
Alisisitiza haja ya ushirikiano kati ya wizara mbalimbali ili kukomesha unyakuzi wa ardhi, uhamishaji usio halali na utapeli wa umiliki wa ardhi.
Akizungumza katika kongamano la usalama lililofanyika kaunti hiyo kama sehemu ya ziara ya Jukwaa la Usalama katika kaunti sita za Pwani, Murkomen alisema matatizo sugu ya umiliki wa ardhi yamekuwa yakichochea migogoro, uhasama na uhamishaji wa watu katika maeneo mbalimbali ya Pwani.
“Katika Kaunti ya Taita Taveta na maeneo mengine ya Pwani, migogoro ya ardhi ni chanzo kikubwa cha machafuko. Tatizo la watu wasio na ardhi, unyakuzi wa ardhi kwa nguvu, na magenge yanayotekeleza amri za uhamishaji bila kufuata sheria limekuwa tishio kwa jamii,” alisema Murkomen.
Aliongeza kuwa baadhi ya magenge haya yanafadhiliwa na watu wenye ushawishi mkubwa, wanaotumia mianya ya kisheria na kupenyeza mfumo wa usajili wa ardhi kwa manufaa yao binafsi.
Waziri huyo alitangaza kuwa serikali imeanza mpango wa mashirika mbalimbali kushirikiana, ikiwemo Wizara ya Ardhi na vyombo vya usalama, ili kushughulikia tatizo hilo la muda mrefu kwa njia ya pamoja.
“Tutaweka mikakati ya kuwachukulia hatua wote wanaojihusisha na uvamizi wa ardhi au kutoa amri za kuhamisha watu bila kufuata utaratibu. Hatuwezi kuruhusu wahalifu kujificha nyuma ya stakabadhi feki au maagizo ya mahakama yasiyo halali,” Waziri alionya.
Kauli hiyo ya Murkomen ilijiri wakati ambapo wakazi wengi wa Taita Taveta wanaishi kwa hofu ya kufurushwa kutoka kwenye ardhi waliyopewa na serikali.
Hali hiyo ilithibitishwa pia na Kamati ya Seneti ya Ardhi, Mazingira na Rasilimali Asilia iliyoongozwa na Seneta Mohamed Faki, ilipotembelea kaunti hiyo kukagua hali ya mambo kufuatia ombi kutoka kwa wakazi wa Mwananchi Settlement scheme katika eneo la Mwatate.
Wakazi hao walieleza kuwa licha ya kupewa hatimiliki na serikali, sasa wanakabiliwa na vitisho vya kufurushwa baada ya mahakama kutoa uamuzi unaompa mwekezaji binafsi umiliki wa eneo hilo hilo mwaka uliopita.
Seneta Faki alieleza wasiwasi wake kuhusu mvutano unaoendelea, akisema hali hiyo inaweza kusababisha machafuko iwapo haitadhibitiwa. Alimhimiza mwekezaji huyo kuwapa nafasi wakazi zaidi ya 1,300 walioko kwenye ardhi hiyo kuendelea na shughuli zao kwa amani wakisubiri uamuzi mwingine wa mahakama.
Aidha, alikosoa Wizara ya Ardhi kwa kutoa hatimiliki bila kufanya uchunguzi wa kina, hali ambayo alisema imechangia mkanganyiko mkubwa na migogoro ya ardhi nchini.
“Hii si mara ya kwanza tunakuja Taita Taveta kwa sababu ya migogoro ya ardhi. Kila tunapokuja ni suala la ardhi. Mchakato wa utoaji hatimiliki lazima uwe wa haki na wazi,” alisema Faki.
Seneta wa Taita Taveta, Jones Mwaruma, naye alisisitiza kuwa ni wajibu wa serikali kuhakikisha kuwa wananchi waliopewa ardhi kihalali wanahifadhiwa dhidi ya madai ya baadaye au usumbufu wowote.
“Tunataka suluhisho la kudumu. Wakazi wa Marungu, Maungu Pipeline, Voi na maeneo mengine wanapaswa kuishi kwa amani bila kuhangaishwa kila mara,” alisema Mwaruma.
Mbali na migogoro ya ardhi, Murkomen aligusia changamoto nyingine zinazochangia ukosefu wa usalama kama vile migogoro kati ya wakulima na wafugaji kuhusu maji na malisho, shughuli za uchimbaji madini kinyume cha sheria, na matumizi mabaya ya leseni za utafiti wa madini.
Alisema serikali itashirikiana na Wizara ya Madini kuhakikisha kuwa utoaji wa leseni unafanyika kwa uwazi na kwa kushirikisha jamii kikamilifu. Pia aliagiza maafisa wa polisi kufuata taratibu sahihi wanapotekeleza sheria za madini ili kulinda maslahi ya wananchi.
Murkomen pia alieleza wasiwasi wake kuhusu changamoto za kijamii zinazoathiri usalama kama vile wanafunzi kuacha shule, ukosefu wa ajira kwa vijana, matumizi ya dawa za kulevya, na ongezeko la ukatili wa kijinsia.
Alisema kuwa Kaunti ya Taita Taveta ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa pakubwa na ukatili wa kijinsia, hasa matukio ya ubakaji, ulawiti na udhalilishaji wa watoto, ambapo wahusika wengi ni jamaa wa karibu.
Serikali, alisema, itaboresha ulinzi wa mashahidi na kuanzisha kampeni za kuelimisha jamii ili kupambana na mila na tamaduni zinazowalinda wahalifu wa ukatili wa kijinsia.
Katika kongamano hilo, maafisa wa polisi walieleza changamoto za kiutumishi ikiwemo makazi duni, uhaba wa usafiri, kucheleweshewa kupandishwa vyeo, na kutumwa katika maeneo magumu kwa muda mrefu.
Murkomen alitangaza sera mpya zitakazoweka kikomo cha miaka mitatu kwa maafisa walioko katika vituo vya pembezoni, akisisitiza kuwa kutumwa katika maeneo ya mbali hakupaswi kuchukuliwa kama adhabu.
“Utumishi katika maeneo ya mbali ni jukumu la kitaaluma na unapaswa kuchangia kukuza taaluma ya afisa huyo,” alisema.
Wakati huo huo, alizindua rasmi Kituo cha Polisi cha Kamtonga kilichojengwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Usalama wa Ndani na Hazina ya Maendeleo ya Maeneobunge (NG-CDF).