![]()
Waziri wa Afya Aden Duale ametoa onyo kali kwa hospitali na maduka ya dawa ya kibinafsi yanayoendesha shughuli zao kinyume cha sheria au kwa njia ya udanganyifu chini ya Mamlaka mpya ya Afya ya Jamii (SHA), akisema kuwa vituo hivyo vitafungwa mara moja na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumza siku ya Ijumaa mjini Voi wakati wa uzinduzi rasmi wa SHA na Mageuzi ya Kidijitali katika sekta ya afya katika Kaunti ya Taita Taveta, Duale alifichua kuwa tayari wizara imezifunga hospitali 1,200 za kibinafsi kote nchini. Alisema hospitali hizo zilianzishwa si kwa lengo la kuhudumia wananchi, bali kuibia SHA kwa madai ya kughushi na uendeshaji haramu.
“Wengine wanawatibu wagonjwa wa nje lakini wanawasilisha madai kana kwamba waliwalaza hospitalini ili kupata malipo ya juu,” alisema Duale, na kuongeza, “Iwapo kituo chochote kitapatikana kikifanya hivyo, kitafutiwa usajili. Na kwa madaktari wanaotumia vibaya PIN zao za idhini, watapokonywa leseni na pia watafungwa.”
Aliweka wazi kuwa daktari ambaye jina lake linaonyesha anatibu wagonjwa katika kaunti moja lakini anajulikana kusajiliwa katika kaunti nyingine, atachukuliwa hatua kali.
“Kama unatakiwa kutibu Voi lakini PIN yako inaonekana Mombasa, utawajibika,” alionya.
Duale, anayejulikana kwa uwazi wake wa kusema mambo moja kwa moja, alisisitiza kuwa hata kama kituo cha afya kinamilikiwa na mwanasiasa au mtu mwenye ushawishi mkubwa, hakitasazwa iwapo kitapatikana kinaiibia sekta ya afya.
“Niko tayari kufanya chochote kulinda afya ya wananchi wa Kenya. Haitakuwa kama kawaida tena,” alisema kwa msisitizo.
Waziri huyo aliwahimiza wananchi kuripoti hospitali na maduka ya dawa yanayokisiwa kuwa ya kihalifu, akifichua kuwa wiki ijayo wizara itatuma wakaguzi kaunti ya Taita Taveta kuanza oparesheni ya kufunga vituo vya afya visivyo halali.
Hospitali zinazolaza wagonjwa zaidi ya uwezo wa vitanda pia zilionywa. Duale alisema, “Hospitali hazipaswi kulaza wagonjwa zaidi ya vitanda walivyo navyo. Ukiwa na vitanda 70, walaze wagonjwa 70 tu,” akasisitiza na kuongeza, “Lazima tulinde heshima na usalama wa raia wetu wanapopata huduma za afya.”
Akizungumzia usajili wa SHA, Duale alisema kuwa taifa limepiga hatua kubwa, ambapo Wakenya milioni 24.4 tayari wamejisajili kwa hiari.
Katika Kaunti ya Taita Taveta, wakazi 159,000 wamejiunga na SHA, na kuifanya kaunti hiyo kushikilia nafasi ya 12 kitaifa na ya tatu katika ukanda wa Pwani nyuma ya Mombasa na Lamu. Duale alisisitiza kuwa usajili unaendelea kwa haki na hakuna anayelazimishwa.
Ili kurahisisha zaidi, wizara imezindua nambari ya USSD *147# inayowaruhusu Wakenya kujisajili kwa urahisi kupitia simu zao.
“Tofauti na NHIF iliyokuwa ikiwahudumia hasa Wakenya wenye ajira rasmi ambao ni asilimia 20 pekee ya wananchi, SHA ni ya kila mtu, wale wasio na ajira, maskini, na wale wa sekta isiyo rasmi. Hakuna anayeachwa nyuma,” alisema.

Aliongeza kuwa tangu SHA ianze kutekelezwa, Kaunti ya Taita Taveta imepokea jumla ya shilingi milioni 165 kupitia SHA, na hivyo kuimarisha utoaji wa huduma za afya.
Duale alieleza kuwa huduma za afya za msingi zinazotolewa katika vituo vya afya vya umma na hospitali za kiwango cha chini sasa ni bure kwa wote waliojisajili katika SHA.
“Hakuna anayepaswa kulazimishwa kulipa,” alithibitisha, akifafanua kuwa malipo yanahusu tu matibabu ya ngazi ya juu na ni kwa wale waliochangia malipo ya bima.
Alikanusha madai kuwa wananchi wanalazimishwa kulipa kiasi kikubwa cha pesa kwa mpigo, akisema kuwa mtu anaweza kuchagua kulipa kila siku, kila wiki, kila mwezi au hata kwa mwaka mzima kulingana na uwezo wake.
Wanawake waliojisajili katika SHA wanalipiwa shilingi 30,000 kwa huduma za kujifungua kwa upasuaji (cesarean), sehemu ya mpango mpana wa kupunguza vifo vya mama wajawazito.
Kwa mwaka huu wa kifedha pekee, serikali imetenga kwa ajili ya huduma za afya ya msingi, zinazojumuisha huduma katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za viwango vya chini.
Katika hafla hiyo hiyo, Duale alitangaza kupelekwa kwa wahudumu wa afya wapya 51 kwa mafunzo kwa vitendo katika Kaunti ya Taita Taveta, wakiwemo madaktari 6, maafisa wa kliniki 9, na wauguzi 36, wote wakigharamiwa na serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Hii ni sehemu ya kundi la kitaifa la wahudumu wa afya wapatao 6,000 waliokusudiwa kuimarisha huduma katika kaunti mbalimbali.
Waziri huyo aliipongeza Taita Taveta kwa hatua nzuri katika sekta ya afya, akisema kuwa kaunti hiyo inaongoza kwa baadhi ya viashiria muhimu vya afya. Kati ya vituo 75 vya afya vya umma vilivyoko kaunti hiyo, ni vinne pekee ambavyo bado havijasajiliwa chini ya SHA.
Kusaidia zaidi SHA kuenea, Duale alihimiza kaunti kuanzisha dawati la SHA katika kila kituo cha afya ili kuhakikisha kuwa wakazi wengi zaidi wanajiunga na kufaidika na mpango huo wa mageuzi.
Duale alielezea histiria fupi kuhusu huduma ya afya kwa wote, akisema kuwa tawala zilizopita chini ya marais Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta zilijaribu kuanzisha mpango huu, lakini haukufanikiwa kikamilifu.
“Mpango huu uliwahi kujaribiwa Kisumu, Isiolo na Machakos lakini haukufua dafu. Tofauti safari hii ni nia ya kisiasa. Rais William Ruto ameihakikisha inafanya kazi kwa kila Mkenya,” alisema.
Gavana wa Taita Taveta Andrew Mwadime, aliyeshirikiana na Waziri kwenye hafla hiyo aliunga mkono SHA na mageuzi ya kidijitali katika sekta ya afya.
“Kama kaunti, tuko tayari kushirikiana na serikali ya kitaifa kufanikisha huduma ya afya kwa wote,” alisema.
Afisa Mtendaji Mkuu wa SHA Dkt. Mercy Mwangangi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya Kidijitali Mhandisi Anthony Lenaiyara pia walihudhuria na wakaunga mkono wito wa uwajibikaji, uadilifu na matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma bora za afya.
Kadri SHA inavyozidi kushika kasi kote nchini, Wizara ya Afya imeweka wazi kuwa haitavumilia ufisadi au uzembe katika sekta hiyo. Wananchi wanazidi kuwezeshwa kupata huduma, na taasisi zinazotaka kuiba kupitia mfumo huo zitakabiliwa na mkono wa sheria.
“Afya si biashara ya kuwawezesha wachache kuwa matajiri. Ni haki ya kila Mkenya. Tutailinda kivyovyote,” alisisitiza Duale.