![]()
Matilda Waleghwa amekabidhiwa rasmi uongozi wa Shirika la Kishushe (Kishushe Ranching Cooperative Society Ltd) katika hafla iliyofanyika mjini Voi siku ya Jumatano, ikiashiria mwisho wa migawanyiko ya miaka mingi iliyokuwa imelemaza shughuli katika shamba hilo lenye utajiri wa madini.
Halfa hiyo iliyofanyika bila pingamizi yoyote, ilihusisha uhamisho wa hati muhimu zikiwemo hatimiliki, muhuri wa shirika na namba za akaunti kutoka kwa mwenyekiti anayeondoka Chombo Shete kwenda kwa uongozi mpya, jambo lililotofautiana kabisa na hali ya awali ambapo makundi pinzani ya wanahisa yalikuwa yakizozana mara kwa mara.
Bi. Waleghwa alitangaza kwamba wawekezaji waliokuwa wameidhinishwa na wanachama sasa wako huru kuanza shughuli zao katika shamba lenye ukubwa wa ekari 60,000, hatua inayotoa matumaini mapya kwa shirika lililokuwa likitikiswa na migogoro ya uongozi iliyohatarisha miradi mikubwa kama ule wa kiwanda cha chuma cha mabilioni ya pesa kinachopendekezwa na kampuni ya Devki Group.
“Mara baada ya makabidhiano haya, wawekezaji wote ambao waliwasiliana na wanachama na wakapewa idhini kufanya kazi ndani ya Shamba la Kishushe wako huru kuanza shughuli zao,” Waleghwa alisema, akiongeza kuwa wawekezaji wawili tayari wameidhinishwa na wanachama na wataanza kazi hivi karibuni.
Aidha, alionya wawekezaji na wanachama dhidi ya kurudia makosa ya zamani yaliyosababisha shirika hilo kuingia katika kesi za kisheria na kampuni za uchimbaji madini.
“Mwekezaji atalazimika kuheshimu sheria na makubaliano watakayofikia na wanachama au uongozi wa Shamba la Kishushe. Hatutaki mambo ya kuvutana tena au kesi zisizo na maana mahakamani,” alisema.
Kwa miaka mingi, Shamba la Kishushe limekuwa kitovu cha migogoro ya uwekezaji, hasa dhidi ya kampuni ya Samruddha Resources Kenya Limited, hali iliyozuia maendeleo katika miradi mingine.
Bi. Waleghwa alifichua kuwa hoteli iliyokuwa ikifanya vizuri ndani ya shamba hilo ililazimika kufungwa kutokana na migawanyiko ya kisiasa ndani ya uongozi wa awali, na akawahimiza wawekezaji kufufua mradi huo.
“Mbali na madini, kulikuwa na hoteli iliyokuwa ikifanya vizuri sana, lakini baadaye ikafa kutokana na changamoto za uongozi. Tunawakaribisha wawekezaji wapya kuwekeza, mradi wafuate sheria za ushirika,” alisema.
Wilfred Mwalimo, katibu mpya wa ushirika huo, alielezea shughuli hizo za kukabidhi uongozi kuwa ya kihistoria kwa kuwa ni mara ya kwanza kufanyika kwa amani bila migogoro kati ya kamati inayoondoka na ile mpya.
“Wawekezaji waliokuwa wameidhinishwa katika mkutano mkuu wa wanachama (AGM) wanapaswa sasa kuanza kazi ili jamii ya Taita Taveta ianze kunufaika,” Mwalimo alisema.
Mwalimo alisisitiza kuwa mchakato wa kuidhinisha wawekezaji wapya utakuwa wazi na wa haki, ambapo tangazo la fursa litatolewa hadharani na wanachama watakuwa na neno la mwisho kabla ya mwekezaji yeyoye kuanza kufanya kazi.
“Kama kamati, tutatekeleza wajibu wetu, lakini uamuzi wa mwisho ni wa mwanachama wa Shamba la Kishushe ambaye atakubali au kukataa mwekezaji kulingana na makubaliano,” aliongeza.
Shirika hilo, lenye utajiri wa madini ya chuma (iron ore) na madini mengine, limevutia wawekezaji wengi kwa miaka mingi, lakini migogoro ya uongozi imekuwa kikwazo kikubwa kutokana na mikataba inayokinzana na hali ya kutoaminika.
Mwenyekiti anayeondoka Chombo Shete aliupongeza uongozi mpya na kuwashukuru wanachama kwa kumpa nafasi ya kutumikia kundi hilo.
“Sasa tuna timu mpya iliyochaguliwa na tunaiunga mkono katika kazi yake,” alisema.
Kwa upande wake, Afisa wa Kaunti wa Kilimo na Ushirika, Dawson Katuu, aliahidi ushirikiano wa serikali ya kaunti na shirika hilo.
“Lengo letu kama kaunti ni kuhakikisha kuna mazingira bora yatakayovutia wawekezaji. Tutakaa nao chini kuhakikisha kila mmoja anapata haki yake ipasavyo,” alisema.
Christine Mwashighadi, Afisa wa Kaunti anayesimamia Ardhi, Mipango ya Miji na Madini, alisema idara yake iko tayari kusaidia shamba hilo katika masuala ya maamuzi na upangaji wa matumizi ya ardhi.
“Hii itarahisisha kazi kwa wawekezaji katika sekta mbalimbali kujua wapi au vipi wawekeze,” alisema.
Ili kuongeza mapato na ukuaji, Bi. Waleghwa alisema uongozi mpya umepanga kuongeza idadi ya mifugona kuanzisha miradi wa unyunyiziaji maji kwa kutumia vyanzo vya maji vilivyopo ndani ya shamba hilo.
Alisisitiza kuwa uwazi utakuwa dira kuu katika uhusiano na wawekezaji, ambapo kila mwekezaji atawasilishwa kwa wanachama kwa ajili ya idhini au kukataliwa kulingana na makubaliano yatakayofikiwa.
Makabidhiano hayo ya amani yameleta faraja kwa wanahisa ambao kwa muda mrefu wameona fursa za maendeleo zikikwamishwa na migogoro ya ndani.
Maafisa wa kaunti waliokuwepo katika hafla hiyo walieleza matumaini kuwa mabadiliko haya ya uongozi yatafungua uwezo wa kiuchumi wa shamba hilo na kuinufaisha jamii pana ya Taita Taveta, mradi tu umoja kati ya shirika, wanachama na serikali ya kaunti udumishwe.
Makabidhiano haya yanachukuliwa kama hatua muhimu kwa Shamba la Kishushe, likijitahidi kufuta sura ya migogoro ya zamani na kujijenga upya kama kitovu thabiti cha uwekezaji kinacholinda maslahi ya wanahisa na maendeleo ya jamii.