Loading

Wabunifu na wasanii vijana wameshauriwa kuacha tu kubuni na kulinda kazi zao, bali wanapaswa kuchukua hatua zaidi ya kibiashara kwa kuuza mawazo yao ili kujipatia nguvu ya kiuchumi, kujenga fahari ya kitaifa, na kupata utambuzi wa kimataifa.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Haki Miliki Duniani katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi siku ya Jumamosi, Katibu Mkuu wa Idara ya Viwanda katika Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda Dkt. Juma Mukhwana alisisitiza kuwa ingawa ulinzi wa haki miliki ni muhimu, biashara ya mawazo hayo ndiyo kipimo halisi cha mafanikio.

Aliwahimiza wabunifu kuelekeza juhudi zao katika kutengeneza bidhaa, nyimbo, na mawazo yenye soko, akisema kuwa mafanikio hayapimwi kwa idadi ya maonyesho waliyohudhuria, bali kwa idadi ya bidhaa walizouza.

“Ikiwa hauuzi ubunifu wako, huo si ubunifu wa maana. Ikiwa hauuzi muziki wako, hiyo si muziki. Kugundua wazo na kutembea nalo kutoka onyesho moja hadi lingine bila kuuza ni kupoteza muda,” alisema Dkt. Mukhwana, akiongeza kuwa, “Tunatumia muda mwingi kutengeneza vitu ambavyo havioni mwanga wa siku. Kipimo cha mafanikio ya wazo lako ni idadi ya vipande ulivyoweza kuuza. Ukishindwa kujibu hilo swali, basi uko katika biashara isiyo sahihi.”

Dkt. Mukhwana alielezea kuwa kuna pengo kubwa katika sekta ya ubunifu nchini Kenya, akisema kuwa licha ya idadi kubwa ya hati miliki na alama za biashara kusajiliwa, chini ya asilimia 10 ndiyo huwekwa sokoni. Alionya kuwa ubunifu usio na nafasi sokoni unaweza kupitwa na wakati ndani ya miaka mitano.

Akihamasisha vijana, alieleza kuwa soko kubwa na linalokua barani Afrika linatoa fursa kubwa kwa wabunifu wa Kenya kupanua biashara zao nje ya mipaka ya nchi. Aliwasihi wabunifu wasifiche vipaji vyao, washirikiane inapohitajika katika masoko na mauzo, na kuhimiza Wakenya kupenda bidhaa na ubunifu wa nyumbani ili kukuza uchumi wa nchi.

“Msifikirie soko la Kenya pekee. Serikali imefungua masoko ya Afrika Mashariki kwa bidhaa zenu — Tanzania, Uganda, Burundi, Rwanda, DRC, Sudan Kusini, Somalia. Na sasa, kupitia Mkataba wa Biashara Huru Afrika, mna soko la zaidi ya watu bilioni 1.4,” alieleza.

Wito huo pia uliungwa mkono na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Haki Miliki Kenya (KIPI) Bw. John Onyango, aliyesisitiza kuwa sekta ya ubunifu, hasa muziki, ina uwezo mkubwa wa kuchangia uchumi.

Onyango alitambua maadhimisho hayo kama hatua muhimu kwa wanamuziki na sekta pana ya ubunifu, akiwapongeza waimbaji, watunzi, watayarishaji na wasambazaji wa kazi za muziki. Alisema haki miliki ni zana yenye nguvu ya kufungua fursa za kiuchumi na kuendesha maendeleo ya taifa.

Alieleza kuwa kumekuwa na mabadiliko chanya ambapo sasa Wakenya wanakumbatia muziki wa ndani zaidi kuliko awali, tofauti na enzi ambapo muziki wa kigeni kama Lingala ulikuwa ukitawala.

Onyango alielezea muziki kama njia muhimu ya mawasiliano, yenye uwezo wa kuathiri tabia na mitazamo ya kijamii, na akatoa mfano wa nyimbo zilizochangia harakati za afya ya umma na siasa. Alisisitiza kuwa muziki una mnyororo mkubwa wa thamani kiuchumi kutoka kwa watunzi hadi kwa wachapishaji, watumbuizaji na watengenezaji wa vifaa, hivyo kuchangia ajira, kipato, na pato la taifa (GDP).

Aliwataka wanamuziki kuchukulia kazi yao kama biashara halisi, si burudani tu, akibainisha kuwa taasisi kama Bodi ya Hakimiliki Kenya (KECOBO) na Mamlaka ya Kukabiliana na Bidhaa Bandia zinafanya kazi kuwalinda na kuhakikisha wanapata mapato stahiki.

“Tazameni muziki kama biashara. Hii si shughuli ya kujifurahisha tu. Tunawahimiza wanamuziki kuutazama muziki kama biashara inayoweza kuwaletea kipato kikubwa,” alisema Onyango.

Katibu Mkuu wa Idara ya Viwanda katika Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda (MITI), Dkt. Juma Mukhwana (wa pili kulia) pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Hati Miliki Kenya (KIPI), Allan Kosgei (wa pili kushoto) wakitangamana na waoneshaji maonyesho wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Miliki Ubunifu yaliyofanyika katika kituo cha mikutano ya kimataifa cha Kenyatta (KICC).

Onyango alisisitiza dhamira ya KIPI kushirikiana na wabunifu vijana ili kuwawezesha, huku akiitaka serikali kuongeza msaada wake ili sekta hii ichangie kikamilifu katika uchumi wa taifa.

Vilevile, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Kukabiliana na Bidhaa Bandia, Dkt. Robi Mbugua, alisisitiza kuwa ubunifu ni kazi ya makusudi, si bahati nasibu.

Alionya kuwa wizi wa kazi za ubunifu na bidhaa bandia ni kosa la jinai na pia ni dharau kwa heshima ya kitaifa. Alifichua kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, oparesheni za kutekeleza sheria zimepelekea kukamatwa kwa vifaa vya muziki bandia vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni thelathini (30).

Dkt. Mbugua alisifu muungano wa KIPI na KECOBO kuwa Mamlaka ya haki miliki ya Kenya, akisema hatua hiyo imeimarisha vita dhidi ya bidhaa bandia. Aliwahakikishia wabunifu kuwa serikali inachukua hatua kuhakikisha kazi zao zinatambuliwa, zinaheshimiwa na wanapata malipo yao.

“Katika kipindi cha miaka mitano, tumekamata vifaa vya muziki bandia ikiwemo spika, ngoma, gitaa na vipaza sauti, vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 30,” alisema Mbugua.

Alisema ubunifu haupaswi kulindwa tu kisheria bali pia kupitia dhamira ya jamii, kwani muziki na sanaa nyingine zina nafasi muhimu katika kufundisha, kuhamasisha, kuponya na kuunganisha watu.

Mwenyekiti wa KIPI Bw. Allan Kosgei aliwakaribisha wageni katika hafla hiyo, akisisitiza umuhimu wa kusherehekea miliki ubunifu kama kichocheo cha maendeleo na uvumbuzi.

Alielezea dhamira ya KIPI katika kuhamasisha shughuli za kidijitali kwa msaada wa Shirika la Haki Miliki Duniani (WIPO), akisema mchakato huo utaboresha uwazi, kasi na ufanisi katika utoaji wa huduma. Alisisitiza kuwa kusaidia wabunifu ni sehemu muhimu ya kufanikisha Ajenda ya Mabadiliko ya Uchumi wa Chini Juu nchini Kenya.

“Tumejitolea kukumbatia ajenda ya serikali ya kidijitali na tunaendelea kuboresha mifumo yetu kwa msaada wa WIPO ili kuharakisha utoaji wa huduma bora,” alisema Kosgei.

Naye Mwenyekiti wa Mamlaka ya Kukabiliana na Bidhaa Bandia, Bw. Josphat Kabeabea, aliwapongeza wabunifu, akieleza kwa mzaha kuwa ingawa mpira wa miguu unapendwa, muziki una nguvu isiyolinganishwa.

Alisisitiza kuwa historia ya Kenya imeelezwa kupitia muziki, ngoma, mashairi na hadithi, sio tu kama urithi wa kitamaduni bali pia kama zana za kisiasa na mali ya kiuchumi.

Kabeabea aliwahimiza wabunge kuchunguza kwa kina ikiwa sheria zilizopo za hakimiliki zinawalinda kikamilifu wabunifu, na akatoa wito wa kuongezwa kwa sheria na bajeti mahsusi kwa sekta ya ubunifu.

Alionya kuwa kupuuzia wabunifu kutaiweka nchi hatarini kupoteza hadithi zake, utamaduni wake na roho yake. Kwa hisia kali, alihimiza kuwa kama Wakenya wanapenda nchi yao, lazima walinde haki za wabunifu, na akaahidi kuwa taifa linasimama pamoja na wasanii kuhakikisha wanafaidika kutokana na kazi zao.

Serikali, kupitia mashirika yake mbalimbali, iliahidi kuendelea kusaidia sekta ya ubunifu na uvumbuzi nchini kwa manufaa ya heshima ya kitaifa na mabadiliko halisi ya kiuchumi.

View all posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

WhatsApp