![]()
Mashindano ya magari ya Equatorial Classic Rally 2025 yameanza rasmi katika Shamba la Teita, eneobunge la Mwatate, Kaunti ya Taita Taveta, Alhamisi asubuhi, yakileta pamoja madereva 19 wakiwemo wanne wa kimataifa.
Tukio hili la siku tatu lililozinduliwa na Gavana wa Kaunti hiyo, Andrew Mwadime na Naibu wake Christine Kilalo, linatarajiwa kuchukua zaidi ya kilomita 628 za barabara zenye changamoto, ndani ya eneo la hifadhi ya binafsi la Teita Estate.
Akizungumza na wanahabari muda mfupi baada ya uzinduzi, Kashif Shaikh ambaye ni mratibu mkuu wa mashindano haya, alithibitisha kuwa mbio zilikuwa zimeanza rasmi huku magari karibu kumi yakiwa tayari yamekamilisha awamu ya kwanza ya mashindano (SS1) kufikia majira ya saa nne asubuhi.
“Mashindano yameanza rasmi. Tulikuwa na madereva 20 waliojiandikisha, lakini mmoja wa kimataifa hakuweza kufika kutokana na changamoto za usafiri. Kwa sasa tuna madereva 19, na leo pekee wanatarajiwa kushindania kilomita 268,” alisema Shaikh.
Miongoni mwa magari yanayovutia ni Mini Cooper ya cc 1300, ndogo kuliko yote katika mashindano haya, inayoweka ladha ya kipekee ya kihistoria katika ushindani huo. Mashindano haya yamevutia mashabiki wa magari kutoka ndani na nje ya nchi, kwa mchanganyiko wa magari ya kizamani na yale yaliyoboreshwa kwa kasi.
Ili kuhakikisha usalama na uratibu wa mashindano, Shaikh alieleza kuwa zaidi ya waamuzi 100 wamewekwa maeneo mbalimbali ya njia, pamoja na magari maalum ya kuokoa yaliyokwama matopeni, huku polisi na walinzi wa wanyamapori kutoka hifadhi jirani wakishiriki kikamilifu.
“Changamoto kubwa kwa sasa ni matope kutokana na mvua zilizonyesha hivi karibuni. Hata hivyo tumejipanga vyema. Tuna magari mawili yanayopita mbele ya magari ya mashindano kukagua njia, na madereva wote wameelekezwa kuwaruhusu wanyama pori kupita wanapokutana nao. Mashindano haya yanafanyika kabisa ndani ya shamba la binafsi, na uhifadhi wa mazingira ni kipaumbele,” akaongeza Shaikh.
Awali mashindano yalipangwa kufunika umbali wa kilomita 800, lakini mvua na barabara kutopitika kulilazimu waandaaji kupunguza kilomita 160, hivyo kufanikisha umbali wa mwisho wa kilomita 628.
Ukaguzi wa kiufundi na usalama wa magari ulifanyika Jumatano, ambapo madereva walifanya mazoezi kujifahamisha na njia na kurekebisha magari yao kabla ya kuanza rasmi.
Gwiji wa mashindano ya magari nchini Kenya, Ian Duncan, ambaye alihudhuria maandalizi ya kabla ya mbio, aliwapongeza waandaaji wakiongozwa na Anthony Nielsen kwa kuandaa tukio la kiwango cha juu katika eneo jipya.
“Ni jambo la kupendeza. Inasikitisha tu kwamba Anthony hatashiriki, bila shaka atatuonea wivu kesho. Lakini wamefanya kazi ya kupigiwa upato. Natumai mashindano haya yataendelea kudumu,” alisema Duncan.
Tofauti na mashindano ya kawaida, Equatorial Classic Rally haina utangulizi wa uchunguzi wa njia (recce) wala nakili za mwendo (pace notes), ikifuata mtindo wa marathon rally ambao hujaribu uwezo wa gari na akili ya dereva.
Tauseef Khan, bingwa wa Afrika kwa upande wa mashindano ya magari, anamsaidia Farhaz Khan katika mashindano haya ya kwanza. Alieleza kuwa mtindo huu wa mashindano unaweza kuwa wa faida kwao.
“Hakuna recce, jambo ambalo huwa changamoto kwa co-drivers. Tayari nimewahi kushindana na Farhaz, hivyo tunafahamiana. Ni suala la kuingiliana kwa haraka, na naamini tutaingiana baada ya kilomita chache,” alisema.
Pia kwenye mashindano haya ni Max Wolstenholme kutoka Uingereza, anayeshiriki kwa mara ya kwanza huku akiongozwa na Victor Okundi mwenye uzoefu kutoka Kenya. Okundi alisema mashindano haya yanahitaji umakini wa hali ya juu, hasa bila kutumia nakili zozote.
“Hili ni tukio la nyumbani kwangu, na Equatorial Classic Rally ni kama familia. Kila kitu kinahusu hali ya kisaikolojia. Tuko tayari,” alisema.
Equatorial Classic Rally inalenga kuwa tukio la kila mwaka katika ratiba ya mashindano ya magari Afrika Mashariki, na mashindano haya yanaashiria mwanzo mzuri.
Mchanganyiko wa changamoto za kiufundi, masuala ya kimazingira, na ushiriki wa kimataifa unaliweka kuwa moja ya mashindano ya kufuatilia kwa makini katika miaka ijayo.
Huku madereva wakionyesha uweledi wao haswa katika kundesha magari kwenye njia zilizojaa changamoto na kwa kasi zaidi, lililosalia sasa ni kuona nani ataibuka mshindi mwishoni mwa mashindano haya.