![]()
Serikali imetangaza kuongeza juhudi za kulipa fidia kwa waathiriwa wa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori na kutekeleza mikakati ya kudumu kama vile kujenga ua za umeme na miradi ya maji ili kukabili ongezeko la visa vya wanyama kuvamia makazi ya watu katika Kaunti ya Taita Taveta na maeneo mengine yaliyoathirika zaidi.
Akizungumza wakati wa hafla ya ulipaji fidia iliyofanyika Alhamisi huko Mwatate, Waziri wa Utalii na Wanyamapori Bi. Rebecca Miano alibainisha kuwa zaidi ya Shilingi bilioni 3.8 zimetengwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuwasaidia wananchi waliokumbwa na uvamizi wa wanyamapori kote nchini.
Alisisitiza kuwa hii ndiyo fedha nyingi zaidi kuwahi kutengwa kwa ajili ya mpango huo tangu kuanzishwa kwake.
“Hii inaonyesha dhamira ya serikali ya Rais William Ruto kutatua changamoto ya migogoro kati ya binadamu na wanyamapori. Tumeweza kupiga hatua kwenye mchakato wa ulipaji fidia, na kwa wale ambao bado hawajalipwa, serikali inashughulikia mchakato huo kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma,” alisema Bi. Miano.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, ni Shilingi bilioni 2 pekee zilizotengwa kwa fidia, ikilinganishwa na zaidi ya Shilingi bilioni 3.8 zilizotolewa ndani ya miaka mitatu pekee.
Mwaka 2023 zilitengwa silingi milioni 906, Shilingi milioni 960 mwaka 2024, huku shilingi milioni 950 zikitengwa kwa mwaka 2025. Aidha, shilingi milioni 800 zimetengwa kwa ajili ya bima na shilingi milioni 250 kwa ajili ya kusaidia kamati zinazoshughulikia madai ya fidia.
Katika Kaunti ya Taita Taveta pekee, wakazi walipokea Shilingi milioni 70 mwaka wa 2024 na Shilingi milioni 45 mwaka wa 2025.
Waathiriwa 22 tayari wamenufaika na ulipaji fidia mwaka huu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii Bi. Sylvia Museiya alisema kuwa serikali ya sasa imeweka kipaumbele kwenye ulipaji wa fidia kwa wakati, tofauti na serikali ya awali ambayo alidai haikutilia maanani suala hilo.
“Utawala huu umeonyesha kujitolea si kwa kutoa fedha pekee, bali pia kuhakikisha mchakato unakuwa wa haraka na wa haki,” alisema.
Pamoja na hatua hizo, viongozi wa eneo hilo walitoa wito wa kuharakishwa kwa mchakato wa fidia. Mbunge wa Mwatate Peter Mbogho Shake na mwakilishi wadi ya Chawia Joseph Mabishi waliitaka wizara kupunguza muda unaochukuliwa kufidia familia zilizoathirika.
“Fomu za fidia zinapaswa kupatikana kwa urahisi kwa wananchi na si katika ofisi za mbali,” alisema Mabishi.
Aidha, alilalamikia ukatili unaofanywa na walinzi wa hifadhi kwa wenyeji wanaopatikana ndani ya mbuga, akisema kuwa wanaokiuka sheria wanapaswa kufikishwa mahakamani badala ya kupigwa.
Kwa upande wake, Mbunge Shake alisema, “Uwekaji wa ua la umeme utasaidia kuzuia wanyama pori wasiingie katika makazi ya watu. Lakini wakati tunasubiri suluhisho la kudumu, tutilie mkazo kuwafariji waathiriwa kwa wakati.”
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini (KWS), Dkt. Erastus Kanga alihakikishia umma kuwa shirika hilo linaendelea kulinda maisha ya watu na wanyamapori kwa pamoja. Alisema Kaunti ya Taita Taveta inashika nafasi ya pili kwa kuathirika zaidi na migogoro kati ya binadamu na wanyamapori baada ya Kajiado, na mbele ya Narok, Laikipia, Meru, Isiolo na Makueni.
Ili kupunguza migogoro hiyo, KWS inajenga ua za umeme maeneo ya Taita Taveta ikiwemo ule wa Bura-Kamtonga-Mgeno na mwingine kutoka Mgeno hadi Sagalla na Kasigau.
“Tunaendelea pia kuchimba mabwawa ya maji ndani ya hifadhi ili kuhakikisha wanyama wanapata maji huko na wasielekee kwenye makazi ya watu,” alisema Dkt. Kanga, huku akimpongeza Rais Ruto kwa kuunga mkono uhifadhi wa wanyamapori na mpango wa fidia.
Alifichua kuwa sekta ya utalii ilipata mapato ya rekodi ya Shilingi bilioni 460 mwaka jana, sehemu ya fedha hizo ikielekezwa kusaidia jamii zilizo karibu na hifadhi.
Naibu Gavana wa Taita Taveta, Bi. Christine Kilalo alitoa wito kwa serikali kuu kuanzisha mfuko wa dharura kusaidia wakazi wanaojeruhiwa na wanyama pori wakati wakisubiri fidia. Alipendekeza pia kufanyiwa marekebisho kwa Sheria ya Fidia ya Wanyamapori ili kujumuisha wanyama wadogo lakini waharibifu kama nyoka, tumbili na nyani.
“Watu wetu wanapoteza mimea na wengine kujeruhiwa na hawa wanyama lakini hawapati fidia kwa sababu hawajajumuishwa kwenye sheria iliyopo,” alisema.
Kilalo pia alitaka kuwe na mgao wa mapato wa asilimia 50/50 kati ya serikali ya kaunti na ya kitaifa kutoka kwa mapato ya utalii wa wanyamapori, na pia kutaka wakazi wa maeneo jirani na mbuga wapewe kipaumbele kwenye nafasi za kazi katika miradi ya uhifadhi.
Waziri Miano alisisitiza haja ya ushirikiano wa karibu kati ya jamii, viongozi wa kisiasa na wizara yake ili kukamilisha madai ya fidia yaliyosalia na kuzuia migogoro ya baadaye.
“Tunahitaji mtazamo wa pamoja. Tusiangalie fidia pekee, bali tuwekeze kwenye suluhisho endelevu linalohakikisha usalama wa watu wetu na wanyama pori,” alisema.