![]()
Gavana wa Kaunti ya Taita Taveta, Andrew Mwadime, ameongoza uzinduzi wa zoezi kubwa la kuchanja mifugo katika kaunti hiyo, likilenga kulinda mifugo na kuibadilisha Taita Taveta kuwa eneo huru lisilo na magonjwa ya mifugo ili kuboresha upatikanaji wa masoko.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Kitaifa wa Chanjo kupitia Mfumo wa E-Voucher kwa ng’ombe, kondoo na mbuzi katika eneo la Manoa, kaunti ndogo ya Mwatate, Gavana Mwadime alieleza kuwa mpango huo ni hatua muhimu katika kujenga sekta ya mifugo imara na yenye faida kubwa kwa wakulima wa kaunti hiyo.
“Hatua hii si kuhusu chanjo pekee, bali ni kuhusu kulinda riziki za wananchi, kukuza biashara na kubadilisha kilimo sambamba na lengo letu la kufanya kilimo kiwe sekta ya kuvutia na yenye tija kwa wakulima wetu wa mifugo,” alisema Gavana Mwadime.
Zoezi hilo la chanjo limeanzishwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Kaunti ya Taita Taveta na Mradi wa National Agricultural Value Chain Development Project (NAVCDP), na linanuia kukabiliana na magonjwa ambayo yamekuwa yakitatiza wafugaji katika eneo hilo.
Ng’ombe watapewa chanjo dhidi ya ugonjwa wa miguu na midomo (Foot and Mouth Disease – FMD), huku kondoo na mbuzi wakipewa kinga dhidi ya ugonjwa wa Peste des Petits Ruminants (PPR).
Gavana Mwadime alisema kuwa Taita Taveta ina uwezo mkubwa wa kuwa soko mahsusi la mauzo ya mifugo nje ya nchi, hasa katika usambazaji wa nyama na bidhaa za nyama. Hata hivyo, milipuko ya magonjwa imeendelea kuwa kikwazo kikuu katika kufanikisha lengo hilo.
Hivi karibuni, kaunti hiyo ilikumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa ngozi ya vinundu (Lumpy Skin Disease) uliyoathiri zaidi ya wanyama 5,000, na kusababisha vifo, kupungua kwa mapato ya wafugaji na kupoteza masoko.
“Milipuko ya magonjwa ya mifugo huathiri sekta kwa njia nyingi ikiwemo kufungwa kwa masoko, matumizi ya mara kwa mara ya viuavijasumu kutibu dalili (ambayo husababisha usugu wa dawa na hatari kwa afya ya umma), gharama kubwa za matibabu, na kupungua kwa faida kwa wakulima wetu wachapa kazi. Ni muhimu sana kuchukua hatua za kinga,” alisema.

Kaunti imeorodhesha zaidi ya wakulima 53,000 wanaoshiriki katika kilimo cha mazao na ufugaji. Kwa mujibu wa takwimu, kaunti hiyo ina ng’ombe 39,740, mbuzi 87,248 na kondoo 12,488 ambao wote wanalengwa katika kampeni ya chanjo.
Kupitia mfumo wa E-voucher, wakulima watapata ruzuku ambapo watalipa Sh50 kwa kila ng’ombe na Sh3 kwa kila mbuzi au kondoo, huku serikali ya kitaifa ikigharamia Sh110 kwa ng’ombe na Sh30 kwa mifugo midogo.
“Tunajivunia kuzindua mfumo huu wa kwanza wa aina yake wa utoaji huduma za chanjo katika kaunti yetu. Kupitia mfumo wa E-voucher, wafugaji wataunganishwa na madaktari wa mifugo walioidhinishwa pamoja na vyama vya ushirika vilivyopo. Hii italeta uwazi, ufanisi na uwajibikaji,” alisema Mwadime.
Mpango huo utatekelezwa kupitia vyama mbalimbali vya ushirika vya wakulima vikiwemo Tagho Dairy FCS, Mwafugha Dairy FCS, Diwadane FCS, Rong’e FCS, na Taita Taveta Banana FCS kwa kushirikiana na wataalamu wa mifugo wa kibinafsi.
Gavana aliwahimiza wakulima wote kujiandikisha na vyama vya ushirika katika wadi zao, akisema kuwa vyama hivyo ni nguzo muhimu za utoaji wa huduma kama chanjo, pembejeo, mafunzo, masoko na mikopo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Uchumi Samawati katika Bunge la Kaunti, Stephen Mkala, alisema mpango wa chanjo utawasaidia sana wakulima ambao hapo awali hawakuweza kuchanja mifugo yao kutokana na gharama kubwa.
“Katika Kaunti ya Taita Taveta tulikuwa tukisafirisha mifugo kwenda Mauritius wakati eneo letu lilipokuwa huru na magonjwa,” alisema Mkala, akiongeza kuwa bunge la kaunti limekuwa likiipa sekta hiyo kipaumbele katika mgao wa fedha za kufadhili miradi.
Waziri wa Kaunti anayesimamia Kilimo, Mifugo na Uchumi Samawati, Dawson Katuu, alisema kuwa kaunti inalenga kuwafikia zaidi ya wakulima 50,000 na zaidi ya mifugo 80,000 kupitia mradi huo.
Alisema mifugo katika kaunti hiyo inakabiliwa zaidi na magonjwa ya mapafu na kuongeza kuwa sheria zimewekwa ili kuimarisha harakati za vyama vya ushirika.

Mwakilishi Wadi, Mabishi Joseph, alikaribisha ushirikiano kati ya serikali ya kitaifa na serikali ya kaunti katika kuwaletea wakulima chanjo kwa bei nafuu.
“Tunafurahia kuwa mradi huu umefika kwa wakati unaofaa, hasa wakati mvua inakaribia kuanza, kwa sababu mara nyingi mvua inaponyesha, ndipo magonjwa ya miguu na midomo pamoja na yale ya mapafu huanza kuibuka,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afya ya Mifugo, Dkt. Jeremiah Ngugi, aliwahimiza wakazi kuunga mkono mpango wa chanjo, akisema ni hatua muhimu katika kufungua masoko ya bidhaa za mifugo.
“Mpango huu utatusaidia kupata masoko ya bidhaa zetu za mifugo kwa sababu nchi nyingi zinazonunua bidhaa zinataka kuhakikisha haziingizi magonjwa kutoka kwa wanyama wetu,” alisema.
Aidha, alisema mpango huo utatoa fursa za ajira kwa vijana waliopata mafunzo katika afya ya mifugo.
Gavana Mwadime aliongeza kuwa mpango huo utakuwa na manufaa mengine, ikiwemo teknolojia ya kuchanganua pua za mifugo kama vitambulisho vya kipekee, sawa na alama za vidole kwa binadamu.
Alisema hatua hiyo itasaidia kukabiliana na wizi wa mifugo kwani kila mnyama ataweza kutambulika kwa urahisi.
Aliwataka wakulima kushirikiana na maafisa wa mifugo na kusajili mifugo yao yote, huku akikanusha uvumi kwamba watatozwa kodi kwa wanyama wao.