Loading

Serikali imeongeza juhudi zake za kupambana na ukatili wa kijinsia na mauaji ya wanawake nchini kupitia mpango wa ushirikishwaji wa umma unaoendelea kote nchini, ukiongozwa na kikosi kazi maalum kilichoundwa na Rais William Ruto mnamo Januari 2024.

Kikosi kazi hicho, kinachojulikana kama Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Ukatili wa Kijinsia na Mauaji ya Wanawake, kikiongozwa na Abdi Washala Mohammed, kilifanya kikao cha hadhara katika eneo la Mwatate, Kaunti ya Taita Taveta siku ya Jumatatu, ambapo manusura, viongozi wa kijamii, na wanaharakati wa haki za kijinsia, asasi za kiusalama walitoa wito wa kuimarishwa kwa sheria, kuongezwa kwa vituo vya uokoaji, na kuanzishwa kwa kampeni za uhamasishaji wa umma ili kukomesha janga hilo linalozidi kuenea.

Kamati hiyo inaendelea na mchakato wa siku 30 kukusanya maoni kutoka kwa wananchi kote nchini ili kuunda mikakati ya kutekelezeka ya kukabili tatizo hili. Kamati hii iliundwa kufuatia kilio cha kitaifa baada ya ongezeko la visa vya ukatili, hasa vinavyolenga wanawake na wasichana.

Washala alifichua kuwa wanawake na wasichana 226 waliuawa mwezi Februari 2024 pekee, ambapo 100 kati yao walikuwa wasichana, akisisitiza uzito na dharura ya hatua ya serikali.

“Hizi si takwimu tu. Haya ni maisha yaliyopotea, familia zilizovunjika, na ndoto zilizokatizwa,” alisema.

Ziara hiyo ya Mwatate ni sehemu ya mchakato wa kamati hiyo katika ukanda wa Pwani, unaojumuisha kaunti za Kilifi, Kwale, Lamu, Mombasa na Tana River.

Washala alisema maoni yanayokusanywa yatachangia moja kwa moja katika kuandaa mpango wa kitaifa wa hatua, ikiwa ni pamoja na mapendekezo ya mabadiliko ya kisheria, mgao wa bajeti, na uanzishaji wa mifumo ya kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia.

Naibu Gavana wa Kaunti ya Taita Taveta, Bi Christine Kilalo, aliipongeza serikali kuu kwa kupeleka kikosi kazi hicho ngazi ya jamii, akisema kuwa hatua hiyo itaimarisha ushirikiano kati ya serikali kuu na ile ya kaunti.

Aliitaka kamati hiyo kutoa mapendekezo ya kuongezwa kwa ufadhili kwa vituo vya uokoaji na huduma za msaada kwa manusura, hasa walioko maeneo ya mashinani.

“Wanawake na wasichana wetu walioko vijijini hawana pa kukimbilia wanapopitia unyanyasaji. Kuanzishwa kwa makazi salama na mafunzo kwa maafisa kuhusu masuala ya kijinsia kutarejesha heshima na hata kuokoa maisha,” alisema Kilalo.

Alieleza kuwa kuna haja kwa serikali zote mbili, ya kitaifa na ya kaunti, kutenga fedha kwa ngazi ya jamii ili kuhakikisha kuwa huduma kwa waathirika zinafika moja kwa moja kwa wananchi.

“Hili ni suala zito ambalo mara nyingi hulizungumziwa kana kwamba ni siasa. Ukweli ni kuwa huduma nyingi zinazohitajika na wananchi zinapaswa kufikishwa hadi ngazi ya familia. Ninapozungumzia ngazi ya jamii, namaanisha vijiji na maeneo ambako watu wanaishi, si tu kutoka Nairobi hadi kaunti,” aliongeza.

Kilalo alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti, akisema kaunti zinahitaji msaada zaidi wa kitaalamu na kifedha ili kuanzisha vituo vya usaidizi kwa manusura wa ukatili wa kijinsia, kutoa msaada wa kisaikolojia, na kuendesha kampeni za uhamasishaji.

Aliitaka pia kamati hiyo kupendekeza mageuzi ya kisheria yatakayoharakisha kesi za ukatili wa kijinsia na mauaji ya wanawake mahakamani, kuongeza adhabu kwa wahalifu, na kulinda mashahidi.

“Bila haki ya haraka, tunahatarisha kuenea kwa ukatili kama jambo la kawaida,” alionya.

Kamishna wa Kaunti, Bi Josephine Onunga, alisema kuwa serikali tayari imeanza kuimarisha mifumo ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia kaunti ya Taita Taveta. Alithibitisha kuwa kila moja ya kaunti ndogo ikiwemo Mwatate, Voi, Taveta na Wundanyi, inaripoti angalau visa 10 vya ukatili kila mwezi, baadhi vikihusisha watoto wachanga wa mwaka mmoja pekee.

Alibainisha kuwa kila kituo cha polisi sasa kina afisa mmoja aliyepewa mafunzo ya kushughulikia masuala ya kijinsia. Hata hivyo, alikiri kuwa bado kuna changamoto ya kutoripoti matukio mengi, hasa kutokana na aibu, hofu, na ukosefu wa imani kwa vyombo vya usalama.

“Serikali inafanya kazi yake, lakini jamii nayo inapaswa kuvunja ukimya,” alisema.

Aliongeza kuwa, “Iwapo mtu anahitaji ulinzi wa mashahidi, tunayo hiyo huduma. Tutazungumza nawe na kuona namna ya kukusaidia. Pindi mtuhumiwa anapokamatwa, utakuwa salama pamoja na familia na jamii.”

Alifananisha ukatili wa kijinsia na “dudu hatari”, akisema kuwa jamii inapoendelea kunyamaza, inajiumiza yenyewe pamoja na watoto wao.

Wakati wa kikao hicho, washiriki kutoka jamii, maafisa wa serikali, vikosi vya usalama, mashirika ya kutetea haki za binadamu, na wawakilishi wa serikali ya kaunti walitoa ushuhuda wa kusikitisha na kutoa hoja muhimu, hasa kuhusu ucheleweshaji wa haki na adhabu ndogo kwa wahalifu wa ukatili wa kijinsia.

Baadhi ya manusura walieleza kukatishwa tamaa kwao na hukumu hafifu au kesi kuachiliwa bila haki kutendeka.

Washala aliwahakikishia wananchi kuwa kamati hiyo inachukua kumbukumbu za malalamiko yote ili kuzijumuisha katika ripoti ya kitaifa.

“Tunachambua vikwazo vyote vya haki. Sheria haina maana ikiwa ipo kwenye karatasi tu na haitekelezwi kwa vitendo kulinda wanyonge,” alisema.

Aliongeza kuwa ukatili wa kijinsia na mauaji ya wanawake unaathiri uchumi wa taifa kwa kiasi kikubwa, akikadiria kuwa Kenya hupoteza zaidi ya Shilingi bilioni 40 kila mwaka kupitia gharama za matibabu, kupotea kwa uzalishaji, na gharama za ulinzi na sheria.

“Vita dhidi ya ukatili wa kijinsia si suala la maadili pekee, bali ni jambo la kiuchumi pia. Tukishindwa kulikabili, tunaweza kupoteza kizazi kizima. Tunaweza kupoteza utu wetu,” alionya.

Kwa mujibu wa Kenya Demographic and Health Survey ya mwaka 2022, asilimia 34 ya wanawake na asilimia 17 ya wanaume wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 49 wameripotiwa kufanyiwa ukatili wa kimwili au kingono. Hata hivyo, wataalamu wanaamini kuwa idadi halisi inaweza kuwa juu zaidi kutokana na aibu na mifumo duni inayowavunja moyo waathirika kutoa ripoti.

Mashirika ya kijamii yalitoa maandiko yaliyoangazia mila potofu, uzembe miongoni mwa vijana wa kizazi cha leo, na mitandao ya kijamii kama kichocheo cha ukatili. Washiriki kadhaa walitaka serikali kudhibiti zaidi maudhui ya mtandaoni na kuanzisha elimu ya usalama wa kidijitali.

Washala alipongeza michango hiyo na kusema itasaidia kuunda mapendekezo ya kitaifa ya kuzuia ukatili wa kijinsia.

“Ninyi wananchi ndio washirika wetu. Tupo hapa kusikiliza, kurekodi na kuchukua hatua,” alisema.

Aliunga mkono wito wa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa kaunti na kusisitiza kuwa kazi ya kamati hiyo itahitimishwa kwa ripoti ya kina itakayowasilishwa kwa Rais.

“Huu si mkutano wa kusikiliza tu bali ni hatua ya kwanza katika harakati ya kitaifa ya uokoaji,” alihitimisha.

Kamati hiyo itaendelea na mikutano ya hadhara katika kaunti nyingine za Pwani wiki hii kabla ya kurejea Nairobi kuandaa ripoti ya mwisho. Inatarajiwa kuwasilisha mapendekezo yake kwa Rais mwezi Juni 2024.

View all posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

WhatsApp