![]()
Serikali ya Kaunti ya Taita Taveta imewataka wafugaji kuchukua hatua za mapema kukabiliana na athari za ukame unaoendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo kwa kuhifadhi malisho, kuhakikisha mifugo inapata lishe bora, maji safi na chanjo dhidi ya magonjwa.
Akizungumza kuhusu hali ya mifugo katika msimu wa kiangazi na baridi, Mkurugenzi wa Afya na Matibabu ya Mifugo katika Kaunti ya Taita Taveta, Dkt. Jeremiah Ngugi, alisema maeneo mengi hasa Voi yanakabiliwa na upungufu wa malisho kutokana na mvua za msimu wa Machi hadi Mei kutokuwa za kuridhisha.

Alisema idara ya mifugo imekuwa ikiwashauri wafugaji kuhifadhi nyasi walizovuna wakati wa mvua ili zitumike kipindi hiki cha ukame. Aidha, aliwahimiza wakulima walio karibu na vyanzo vya maji kupanda mazao ya malisho kama nyasi aina ya Napier na mahindi kwa ajili ya kuhifadhi chakula cha mifugo.
“Tumeshauriana na wakulima jinsi ya kuhifadhi malisho ya mifugo. Kuna wale ambao wako katika sehemu karibu na mito wanaeza kufanya upanzi wa nyasi kama Napier ili kuhifadhi kwa wakati kama huu,” alisema daktari.

Daktari Ngugi alieleza kuwa uzalishaji wa maziwa hupungua wakati wa ukame kutokana na upungufu wa malisho, hivyo wafugaji wa ng’ombe wa maziwa wanapaswa kuongeza virutubisho na chakula cha ziada (supplementation) ili kudumisha uzalishaji.
“Uzalishaji wa maziwa umepungua sababu ya kiangazi. Tunahimiza wafugaji kuwapa chakula cha ziada wanyama wao ndio uzalishaji wa maziwa usipungue sana wakati huu,” alisema.

Pia aliwataka wafugaji kuzingatia afya ya mifugo yao, akisema kipindi cha ukame husababisha wanyama kuhamishwa kutoka eneo moja kwenda jingine kutafuta malisho na maji, hali inayoongeza hatari ya kusambaa kwa magonjwa.
Alibainisha kuwa ugonjwa unaotia wasiwasi zaidi kwa sasa ni wa miguu na midomo (Foot and Mouth Disease), huku akieleza kuwa serikali ya kaunti inaendelea na kampeni ya chanjo katika maeneo ya Kasigau. Aidha, alisema mbuzi na kondoo pia wanachanjwa katika maeneo ya Mbololo, Ngolia na Kishushe ili kuwakinga dhidi ya magonjwa mbalimbali.

“Ugonjwa unaotupa wasiwasi zaidi wakati huu wa kiangazi ni ugonjwa wa miguu na mdomo. Tunaendeleza chanjo katika sehemu za Kasigau, na pia tunachanja mbuzi na kondoo katika sehemu za Mbololo, Ngolia na Kishushe ili tuhakikishe wakulima wanaweka wanyama wao katika afya njema,” alisema Dkt. Ngugi.
Kwa mujibu wa Dkt. Ngugi, ukame pia umesababisha ongezeko la visa vya magonjwa ya mapafu kwa mbuzi kutokana na msongo unaotokana na upungufu wa malisho. Aliwahimiza wafugaji kutoa taarifa mapema kwa maafisa wa mifugo wanapoona dalili za magonjwa ili hatua za haraka zichukuliwe.

“Tumekuwa na shida ya ugonjwa wa mapafu ya mbuzi nan i vizuri wakulima waweze kutoa habari kwa madaktari wa afya ambao wako nyanjani kama kuna changamoto kama ile ili tuweze kudhibiti.”
Mbali na ufugaji wa ng’ombe na mbuzi, Dkt. Ngugi aliwashauri wakulima kuwekeza katika ufugaji wa kuku wa kienyeji, akisema ni mradi unaohitaji malisho machache na unaweza kuwa chanzo kizuri cha kipato wakati wa ukame.
“Ni vizuri wakulima kuangazia ufugaji wa kuku za kienyeji kwa sababu wanafanya vizuri sana katika sehemu hii na wakati huu ambapo malisho ni haba na pia hawahitaji malisho mengi,” alisema.

Alisema kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo, idara ya mifugo imekuwa ikiwafundisha wakulima namna ya kutengeneza lishe mbadala ya mifugo na kulima mmea wa Azolla, ambao una protini nyingi na hutumika kuongeza virutubisho kwa kuku pamoja na mifugo mingine.
Dkt. Ngugi pia alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mifugo inapata maji safi na ya kutosha, akieleza kuwa zaidi ya asilimia 60 ya uzalishaji wa maziwa hutegemea upatikanaji wa maji ya kutosha.
“Asilimia sitini ya maziwa inayokamuliwa inatokana na upatikanaji mzuri wa maji safi. Ni vizuri tuweze kuhakikisha kwamba wanyama wetu wanapata maji ya kutosha na safi.”

Kuhusu uhamishaji wa mifugo, alisema tayari kuna idadi ndogo ya wafugaji kutoka maeneo ya Voi wanaohamisha mifugo wao kuelekea maeneo yenye malisho mengi zaidi kama Taveta na maeneo ya Taita yaliyopata mvua nzuri. Aidha, alisema kuna mifugo kutoka kaunti jirani na maeneo ya Kaskazini Mashariki inayoingia Taita Taveta kutokana na hali bora ya malisho iliyopo.
Alifafanua kuwa Serikali ya Kaunti inashirikiana na vyombo vya usalama kuhakikisha mifugo yote inayohamishwa inakaguliwa na madaktari wa mifugo na kuwa na vibali vinavyohitajika ili kuzuia kusambaa kwa magonjwa ya mifugo.
“Tumeona wanyama ambao wamekua wakitoka kutoka kaunti zingine wakiingia sababu kulinganisha hali ya anga ya Taita Taveta na kaunti zingine kama kule kaskazini mashariki tunaweza kuwa tuko na hali bora zaidi kuwashinda. Kwa hivo tumeona harakati za wanyama kuingia katika kaunti hii. Na kama serikali ya kaunti tumekua tukishirikiana na idara za kiusalama wale ambao wanafanya utekelezaji wa kuhamisha mifugo ndio tuhakikishe wale mifugo ambao wanaingia wameweza kukaguliwa na madaktari wetu na wako na stakabathi ambazo zinafaa ndiyo wasiweze kusambaza magonjwa,”alisema Dkt. Ngugi.

Dkt. Ngugi alihitimisha kwa kuwataka wafugaji kuanza kutekeleza mbinu za uchukuaji wa kimkakati (strategic offtake), ambapo hupunguza idadi ya mifugo kwa kuuza baadhi ya wanyama mapema kabla hali ya ukame haijawa mbaya zaidi, hatua ambayo husaidia kulinda afya ya mifugo iliyobaki na kupunguza hasara kwa wafugaji.